Ufalme wa Mungu

Ufalme wa Mungu (kwa Kiebrania: מלכות malkut, kwa Kigiriki: βασιλεία τοῦ theoũ, basileia tou theou) ni istilahi ya Biblia inayomaanisha kazi ya YHWH (Mungu wa Wanaisraeli) katika Dunia na pia upeo ambamo mapenzi yake yanatimizwa.

Neno hili linafungamana na cheo cha "mfalme" kinachotumiwa kwa YHWH katika Tanakh (Biblia la Kiebrania). Linaonyesha imani kwamba Mungu anatawala juu ya vyote tangu uumbaji na pia kwamba mapenzi ya Mungu yatatekelezwa kote katika siku ya mwisho dhidi ya upinzani wote. Kwa hiyo manabii katika Biblia na maandiko ya kiufunuo huhusisha neno hilo na mawazo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Torati kote duniani, ukombozi wa Wanaisraeli wote kutoka utawala wa kigeni na ukombozi wa mataifa yote kutoka kwa udhalimu, kuja kwa Mungu kwenye hukumu ya mwisho, na mabadiliko ya uumbaji ambayo yatashinda uovu wote pamoja na mateso, maumivu na kifo.

Kulingana na Agano Jipya, Yesu wa Nazareti alitangaza ufalme huu wa Mungu kuwa umekaribia ( Marko 1,15 ). Wanafunzi wake waliona ufalme kwanza katika matendo, kama vile uponyaji wa magonjwa, na mafundisho ya Yesu mwenyewe.

Wakristo wa kwanza waliona kwamba ufalme wa Mungu ulifika katika kazi, kifo na ufufuko wa Yesu. Waliamini kwamba matabiri ya manabii ya Biblia (mfano Isaya 25,8) yalithibitishwa na kuanza kutimizwa katika historia ya Yesu. Maandiko kama Ufunuo 21: yanaonyesha imani hiyo.

Madhehebu ya Ukristo leo yanatofautiana sana katika kuelewa na kueleza mada hiyo.


© MMXXIII Rich X Search. We shall prevail. All rights reserved. Rich X Search